Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Azindua mradi wa ukarabati wa Bwawa la Nyangokolwa

Imewekwa: 07 August, 2026
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Azindua  mradi wa ukarabati wa Bwawa la Nyangokolwa

Zaidi ya wananchi 3,000 wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu wanatarajia kunufaika na huduma ya uhakika ya maji baada ya Serikali kuzindua mradi wa ukarabati wa Bwawa la Nyangokolwa wenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 1.012.

Mradi huo umezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha, huku usimamizi wa utekelezaji ukifanywa na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria kupitia wataalamu wake.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Macha ameipongeza Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria kwa usimamizi mzuri wa rasilimali za maji na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mabwawa katika Mkoa wa Simiyu, akieleza kuwa miradi hiyo inaendelea kuboresha maisha ya wananchi.

Aidha, amewataka wataalamu kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa na kwa viwango vinavyotakiwa, huku akisisitiza kuwa ataufuatilia kwa karibu hadi utakapokamilika.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhe. Mathew Kundo, amesema ukarabati wa Bwawa la Nyangokolwa utakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi kupitia upatikanaji wa maji kwa shughuli za kilimo, umwagiliaji na ufugaji.

Ameeleza kuwa mradi huo ni matokeo ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji.

“Sisi wananchi wa Nyangokolwa tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa ukarabati wa bwawa hili. Mradi huu utaondoa changamoto ya uhaba wa maji na kuboresha maisha ya wananchi,” amesema Mhe. Kundo.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Renatus Shinhu, amesema baada ya kukamilika, bwawa hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 12 za maji, na kunufaisha zaidi ya wananchi 3,000 pamoja na mifugo zaidi ya 5,000.

Dkt. Shinhu ameahidi kuwa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria itasimamia utekelezaji wa mradi huo kwa weledi ili ukamilike kwa wakati na kuzingatia viwango vyote vya ubora vinavyotakiwa.

Wananchi wa Nyangokolwa waliohudhuria uzinduzi huo wameishukuru Serikali kwa kuanza ukarabati wa bwawa hilo, wakisema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji uliowaathiri katika matumizi ya nyumbani, shughuli za uzalishaji na ufugaji, hali iliyowalazimu kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Uzinduzi wa mradi huo umehudhuriwa na viongozi kutoka Wizara ya Maji, Mkoa wa Simiyu, Wilaya ya Bariadi, wataalamu wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria pamoja na wananchi wa eneo hilo, ambao wameeleza matumaini makubwa kuwa mradi huo utaleta suluhisho la kudumu la upatikanaji wa maji na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Wilaya ya Bariadi.